Serikali yaanzisha madawati ya ulinzi kwa watoto mashuleni
30 March 2021, 2:21 pm
Na. Yussuph Hans
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kuratibu uanzishwaji wa madawati ya Ulinzi kwa Watoto katika shule za msingi na sekondari Nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) kwa kipindi Cha Julai,2020 hadi Februari, 2021.
Dkt. Gwajima amesema hadi kufikia Februari,2021 jumla ya madawati 182 yameanzishwa na jumla ya wasimamizi wa madawati shuleni wapatao 360 walipatiwa mafunzo ya namna ya kusimamia madawati hayo ili kupunguza ukatili wa Watoto shuleni.
Amesema katika kutokomeza mila na desturi zenye madhara zinazosababisha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto Nchini, Wizara imetoa elimu kuhusu athari za Mila hizo kwa Watoto, wananchi, walimu pamoja na viongozi wa kisiasa, dini na wale wa kimila katika Mikoa ya Mara,Geita,Tanga,Rukwa,Mbeya na Kigoma.
Kwa upande wa kutokomeza mimba za utotoni Dkt. Gwajima amesema wameweza kuwafikia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuwapatia uelewa kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni kiafya, kielimu na kiuchumi pamoja na kuzuia ukatili mtandaoni.
Katika hatua nyingine ya taarifa ya utekelezaji wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii hususan katika kuwawezesha Wanawake kiuchumi Dkt.Gwajima amesema kupitia Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 pamoja na mkakati wake wa utekelezaji wa mwaka 2005, katika kipindi Cha mwaka 2015 hadi 2020 kiasi cha shilingi Trioni 2.22 zimetolewa Kama mikopo na kunufaisha vikundi vya wanawake wajasiriamali takribani 490,000 vyenye wanawake zaidi ya milioni 4.9.
Alisema mikopo hiyo imetolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) kwa fedha zilizotengwa kupitia vyanzo vya ndani vya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake(4%), vijana (4%) na watu wenye ulemavu (2%).