Wakazi wa mtaa wa nduka walalamikia ubovu wa miundombinu ya maji taka
18 May 2021, 9:02 am
Na; Benjamin Jackson
Mtaa wa Nduka katika Kata ya Chamwino jijini Dodoma unakabiliwa na ubovu wa miundombinu ya maji taka yanayotiririka katika maeneo ya watu.
Wananchi wa eneo hilo wameiambia Dodoma fm kuwa hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara na kusababisha usumbufu kutokana na maji hayo kutoa harufu mbaya.
Wameiomba Serikali ya Mtaa na Kata kuwatatulia kero hiyo ili kuwanusuru na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababishwa na maji hayo.
Akijibu malalamiko ya wananchi hao mwenyekiti wa mtaa wa Nduka Bw.Mohamed Pampayi amesema kuwa wamekuwa wakiitafutia ufumbuzi changamoto hiyo kwa kuwatoza faini wananchi wanaochafua mitaro kwa kutupa uchafu na kuzuia maji kutiririka na kuziba.
Aidha ameongeza kuwa katika mtaa wa Nduka barabara nyingi hazina mitaro hivyo ameiomba Serikali kuipatia ufumbuzi ili kuwaepusha wananchi na adha hiyo.