Madereva wa Bodaboda wahamasisha vijana kujiajiri
9 March 2023, 3:46 pm
Madereva wa Bodaboda wilayani Bahi Mkoani Dodoma wamesema kazi wanayoifanya ni kazi rasmi na kuwahamasisha vijana wasio na ajira kuacha kukaa vijiweni bali watafute hata kazi ya bodaboda ili wajikimu kimaisha.
Na Benard Magawa.
Madereva wa Bodaboda wilayani Bahi Mkoani Dodoma wamesema kazi wanayoifanya ni kazi rasmi inayoingiza kipato halali kama kazi zingine na kuwahamasisha vijana wasio na ajira kuacha kukaa vijiweni bali watafute hata kazi ya bodaboda ili wajikimu kimaisha.
Hayo yamesemwa na madereva wa bodaboda kituo cha Sheli wilayani Bahi walipokuwa wakizungumza na kituo hiki mapema Februari 9 mwaka huu, wamesema ni kweli zipo changamoto katika kazi hiyo lakini ni za kawaida ambazo zipo hata katika kazi zingine.
Wamesema boda boda zinawawezesha kupata mahitaji ya kila siku ikiwa ni tofauti kabisa na kukaa bila kazi yoyote na kuwaepusha kwenye makundi hatarishi yakiwemo ya uhalifu huku zikiwasaidia kujiletea maendeleo katika familia zao.
“ Boda boda ni kazi kama kazi zingine na zinasaidia sana vijana kujikimu kimaisha sababu wengi hatuna ajira za ofisini, lakini kwa sasa tuna uhakika wa kupata mahitaji muhimu ya kila siku kupitia kazi yetu hii ya kusafirisha abiria kwa pikipiki.” Amesema Yohana Blezi
Kwa upande wake Mkapa John Njoliba amesema kuna tofauti kubwa kati ya kijana aliyejiajiri kuendesha bodaboda na yule anayekaa kijiweni kusubiri ajira za serikali kwani hawezi kupata mahitaji yake ya kila siku kwa kukaa vijiweni.
Vijana wasisubiri kuajiriwa wakiwa vijiweni, wajishughulishe na vitu mbalimbali ikiwemo kazi ya bodaboda kwani kikubwa ni kuweza kujihudumia mwenyewe mahitaji yako muhimu
“Vijana wasisubiri kuajiriwa wakiwa vijiweni, wajishughulishe na vitu mbalimbali ikiwemo kazi ya bodaboda kwani kikubwa ni kuweza kujihudumia mwenyewe mahitaji yako muhimu kwa nguvu yako kuliko kukaa kijiweni na kuombaomba huku ukiwa na nguvu na afya njema.” Amesema
Amesema vijana wasomi wasiogope kufanya kazi hiyo kwani hakuna fedheha kubwa kama msomi kushindwa kujiajiri na kujihudumia mwenyewe sababu elimu walizopata zinapaswa kuwasaidia katika kujiletea maendeleo na siyo kuwa tegemezi.
Ikumbukwe kuwa pamoja na changamoto nyingi zinazoelezwa kuhusu kazi hii, kwa miaka ya hivi karibuni usafiri wa pikipiki umejipatia umaarufu mkubwa katika ukanda huu wa Afrika mashariki na kuwawezesha maelfu ya vijana kujiajiri wakiwemo wasomi na kupunguza kwa kiasi kikubwa wimbi la vijana wasio na ajira.