Migogoro ya Ardhi Chemba yapungua kwa kiasi kikubwa
9 July 2021, 12:01 pm
Na; Benard Filbert.
Imeelezwa kuwa migogoro ya ardhi katika Kata ya Chemba Wilayani Chemba Mkoani Dodoma imepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na awali ambapo ilikuwa ikileta ugomvi kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw. Bashiru Athman wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu hali ilivyo katika kutatua migogoro ya ardhi katika eneo lake.
Bwana Bashiru amekiri kuwa awali kulikuwa na migogoro ardhi katika kijiji hicho kutokana na eneo hilo kuwepo makao makuu ya Wilaya ya Chemba.
Amesema kama kiongozi wa kijiji cha chemba amehakikisha migogoro inaisha na kufikia mwafaka.
Licha ya baadhi ya maeneo kuwa na changamoto ya wananchi kuuziwa kiwanja kimoja zaidi ya watu wawili Bw. Bashiru amesema katika kijiji chake hakuna suala hilo kutokana na uelewa wa wananchi kuongezeka.
Yusuph Ally ni mkazi wa kijiji cha chemba ameiambia taswira ya habari kuwa hivi sasa hakuna migogoro ya ardhi kama awali kutokana na umakini wa viongozi wa serikali.
Migogoro ya ardhi ni miongoni mwa changamoto kubwa nchini ambayo imekuwa ikiibua sura mpya kila kukicha huku serikali ikijitahidi kuja na mbinu mpya za kusuluhisha.