Hotuba ya Rais Samia yawapa faraja wananchi
7 April 2021, 1:28 pm
Na; Mindi Joseph
Wakazi Mkoani Dodoma wamesema kupitia Hotuba ya Mh Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyoitoa jana wakati akiapisha viongozi mbalimbali wa kiserikali imewapa faraja na matumaini makubwa katika kutetea haki za wanyonge na watanzania kwa ujumla.
Hayo wamebainisha wakati wakizungumza na taswira ya habari juu ya tathimini yao ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo wamesema hotuba hiyo imegusa kila nyanja muhimu ambazo zitachochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wananchi.
Wameongeza kuwa mengi yaliyowagusa ikiwemo wananchi kupewa fursa ya kuelezea changamoto zao kupitia mabango, kushughulikia suala la korona pamoja na watanzania kutakiwa kufanya kazi kwa bidii.
Aidha wamesema kuwa hotuba yake imejenga dhana ya uwajibikaji bora kwa wananchi na kubadilisha mitazamo ya baadhi ya wananchi waliokuwa na hofu ya Rais huyo kutoweza kusimamia vyema maendeleo ya taifa.
taswira ya habari imezungumza na mchambuzi wa masuala ya kisiasa mohammed jawadu, ambaye amesema kuwa hotuba ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan imetoa taswira chanya kwa utendaji kazi wake na kuongeza kuwa suala la uongozi halichagui jinsia.
Kupitia hotuba yake Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan aliyoitoa jana wakati akiapisha viongozi mbalimbali alizungumza kuhusu masuala mbalimbali katika kuhakikisha viongozi hao wanawajibikia vyema watanzania.