Wananchi waomba maboresho soko la kimataifa Kibaigwa
30 May 2023, 4:29 pm
Soko la kimataifa la Kibaigwa ni utambulisho wa wilaya ya Kongwa kimataifa hivyo lazima litunzwe kama chanzo cha mapato.
Na Bernadetha Mwakilabi.
Wafanyabiashara wadogowadogo katika soko la mazao la kimataifa la Kibaigwa wilayani Kongwa wameiomba serikali kufanya maboresho ya kisasa katika soko hilo ili kukuza biashara na kuvutia wateja wengi zaidi kutoka nje ya nchi.
Wakiongea sokoni hapo wafanyabiashara hao wamesema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukosa mitambo ya kusafishia mazao ambapo kwa sasa wanatumia chekeche za mikono ambazo zimechakaa na zina mgogoro baina ya wafanyabiashara na uongozi wa soko hilo.
Akitolea ufafanuzi suala hilo Afisa Biashara wa soko hilo Bwana Luig Mbuya amesema kuwa uongozi wa soko na wafanyabiashara walikubaliana kuwa chekeche hizo zinunuliwe na kugawiwa Kwa makundi ya wafanyabiashara na endapo zitachakaa basi wanakikundi watazirekebisha, suala ambalo wafanyabiashara hao hawakutekeleza.
Aidha mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel amesema kupitia Hali hiyo Kuna haja ya uongozi wa soko kukutana mara Kwa mara na wafanyabiashara hao ili kujua changamoto zao na kuzitatua mapema.
Hata hivyo Mwema ameonesha kutoridhishwa na mchakato wa usafishaji mazao sokoni hapo na kuongeza kuwa Soko la kimataifa la Kibaigwa ni utambulisho wa wilaya ya Kongwa kimataifa hivyo lazima litunzwe kama chanzo Cha mapato.
Kwa upande wake Kaimu meneja wa soko la kimataifa la Kibaigwa Bwana Athman Nzenga amekili kuwepo kwa changamoto za uchakavu wa miundombinu ikiwemo mitambo ya kusafishia mazao, ukosefu wa uzio na Kamera za ulinzi zitakazosaidia kudhibiti upotevu wa mapato.
Hata hivyo Nzenga ameongeza kuwa Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mapato ya soko hilo yalikuwa milioni 900 na mwaka 2022/2023 mwezi machi yalikuwa milioni 928 na kwamba mapato yanaongezeka mwezi June Hadi disemba msimu wa mavuno ya mazao ya mahindi alizeti Karanga na mbaazi.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kongwa Bwana Fortunatus Mabula amesema kuwa ofisi ya Mkurugenzi ina taarifa ya changamoto hizo na ipo kwenye hatua za utekelezaji.