DC. Gondwe na kampeni ya kuku Robo matibabu mwaka mzima
20 February 2023, 12:29 pm
Kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma zote muhimu zikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, huduma za maabara, huduma ya Mionzi, upasuaji kwa wajawazito na upasuaji wa kawaida, huduma za watoto njiti ambazo hapo awali wananchi walilazimika kuzifuata Dodoma mjini,
Na Benard Magawa
Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe ameiagiza kamati ya usimamizi wa huduma za afya wilaya ya Bahi (CHMT) kuhakikisha wanawahamasisha kikamilifu wananchi kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa (iCHF) ili kujihakikishia huduma za matibabu kipindi wanapopatwa na maradhi.
Gondwe ameyasema hayo Februari 16,2023 alipofanya ziara kwa mara ya kwanza katika hospitali ya Wilaya ya Bahi na kujionea namna huduma zinavyotolewa kituoni hapo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea taasisi zote zinazotoa huduma wilayani humo ikiwa ni wiki mbili tangu alipowasili wilayani hapo baada ya uteuzi mpya wa wakuu wa wilaya uliofanyika hivi karibuni.
“Niwapongeze Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Bahi na timu nzima ya wataalamu, mna hospitali nzuri yenye hadhi na majengo ya kutosha yenye ubora unaokubalika, jitahidini kutoa hutuma zinazoendana na ubora wa majengo haya kwani serikali imewaamini na imetumia fedha nyingi kuwekeza hapa kwenu.” Amesema Gongwe.
Amewaasa wananchi wa Bahi kujiunga kwa wingi katika mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa ya shilingi elfu 30 kwa watu sita sawa na shilingi elfu 5 kwa mtu mmoja gharama inayofanana na kununua kuku robo ambapo kwa kuungana watu sita wa familia moja, marafiki au wanafunzi wenye elfu 5 kila mmoja, wanakuwa na sifa ya kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa itakayowahakikishia matibabu kwa mwaka mzima.
Akizungumzia kuhusiana na kukosekana baadhi ya dawa muhimu katika hospitali hiyo Gondwe amemuagiza Mfamasia wa wilaya hiyo kuhakikisha anaagiza dawa kwa wakati na kuelekeza kufunguliwa kwa duka la dawa la Hospitali ili dawa zinazokosekana katika dirisha la dawa zipatikane dukani kuwaondolea adha ya wagonjwa kukosa dawa wakiwemo wateja wa bima ya afya, na kusema kuwa kwakufanya hivyo kutawavuta wananchi wengi kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa.
“ Kumekuwa na malalamiko ya wagojwa kuhusiana na baadhi ya wahudumu kutokuwajibika ipasavyo, naomba niseme kuwa si wahudumu wote wana matatizo, ni asilimia ndogo tu ndiyo inayochafua tawsira nzuri ya idara ya afya, nikuagize Mganga mfawidhi kuhakikisha kila mtumishi anavaa kitambulisho muda wa kazi ili tuweze kubaini wanaolalamikiwa na wagonjwa na tuchukue hatua dhidi yao.” Amesema Gondwe.
Katibu wa chama cha Mapinduzi Wilaya ya Bahi Bi. Jamila Mjungu akizungumza katika ziara hiyo ameeleza namna watumiaji wa huduma katika hospitali hiyo wanavyowalalamikia baadhi ya wahudumu kutokuwa waadilifu wawapo kazini kwa kutoa lugha zisizoridhisha kwa wagonwa pindi wanapowahudumia pamoja na kukosekana baadhi ya dawa muhimu na kuagiza serikali kuhakikisha watumishi wanaowasimamia wanatekeleza wajibu wao kikamilifu kwa mujibu wa ilani ya chama cha Mapinduzi.
Awali akisoma taarifa ya hospitali kwa Mkuu wa wilaya ya Bahi, mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Bahi Dr. Kasimu kolowa amesema kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma zote muhimu zikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, huduma za maabara, huduma ya Mionzi, upasuaji kwa wajawazito na upasuaji wa kawaida, huduma za watoto njiti ambazo hapo awali wananchi walilazimika kuzifuata Dodoma mjini, pamoja na huduma zote muhimu kwa ngazi ya hospitali na kutoa rai kwa wananchi wa Bahi kuendelea kupata huduma hospitalini hapo.