Dodoma FM

TACAIDS yaidhinishiwa pesa kwaajili ya miradi ya maendeleo.

29 July 2022, 1:43 pm

Na; Alfred Bulahya.

Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania TACAIDS imeidhinishiwa na Bunge Shilingi Bilioni kumi na nne, milion mia tisa themanini na moja laki mbili na ishirini na nne, (14,981,224,000.00) kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika shughuli za matumizi ya kawaida na maendeleo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene wakati akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu vipaumbele vya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu na tasisi zake kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema Shughuli zitakazotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni pamoja na kuratibu upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI kwenye Mikoa ya Iringa, Kagera, Katavi, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Dodoma, Geita, Tabora na Songwe pamoja na kuweka kipaumbele katika kuzuia maambukizi ya VVU kwa vijana wa miaka 15 – 24.

Ameongeza kuwa Katika mwaka wa fedha 2022/23 Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini imeidhinishiwa Shilingi 11,974,701,000.00 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ukilinganisha na kiasi cha Shilingi 8,529,797,000.00 kilichoidhinishwa mwaka wa fedha 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 28.8.

.

Kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo amesema wanaendelea na ujenzi wa kiwanda cha kupiga chapa cha Serikali ambacho kutaisaidia Serikali kulinda usalama wa nyaraka za serikali huku ikiendelea na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Maafa ambacho kitatumika kupokea na kutuma taarifa mbalimbali za Maafa.