Wanawake wa kijiji cha Chambogo Rorya wakabiliwa na mfumo dume unao wanyima haki ya kumiliki ardhi.
11 October 2021, 12:11 pm
Na; Pius Jayunga.
Wanawake jamii ya Kijaruo katika Kijiji cha Chambogo Wilaya ya Rorya Mkoani Mara wanakabiliwa na changamoto ya mfumo dume ambao unawaathiri kimaendeleo kwa kunyimwa haki ya umiliki wa ardhi.
Dodoma FM imezungumza na mmoja wa wanawake katika Kijiji hicho Bi. Rebecca Kagose katika kufahamu namna ambavyo wanawake wanashirikishwa katika umiliki wa mali ikiwemo ardhi katika ene hilo.
Bi. Rebecca amesema jamii ya Kijaruo imemthamini zaidi mtoto wa kiume na kumtelekeza mtoto wa kike kwa madai kuwa akipata elimu pamoja na kumilikishwa ardhi atakwenda kunufaisha upande wa mume wake utamaduni ambao umeendelea kuwaathiri zaidi wanawake hao.
Bw. Silvester Owino kutoka Kijiji cha Kitembe Wilayani Rorya amesema mtoto wa kike ni mali ya mume atakae muoa hapo baadae na hivyo haitakuwa rahisi kuachana na utamaduni wa kuto kumrithisha ardhi mtoto wa kike kwani mali zote za familia ziko chini ya urithi wa watoto wa kiume.
Diwani wa Kata ya Kitembe Bw. Jofrey Samwel akizungumzia swala hilo amesema ni kutokana na jamii ya wajaruo kuto kupatiwa elimu juu ya umuhimu wa mwanamke kurithishwa ardhi kwa maendeleo na hivi sasa maafisa ustawi wa jamii wameanza kutoa elimu ili kumkomboa mtoto wa kike katika swala la umiliki wa ardhi.