Kwa mujibu wa UNICEF silimia 70 ya watoto wa kike Duniani kote wamewahi kupitia aina fulani ya ukatili
6 September 2021, 11:31 am
Na; Fred Cheti.
Takwimu kutoka shirika la kuhudumia watoto Duniani UNICEF zinaonyesha kuwa takriban watoto wa kike wenye umri wa miaka 15 na 19 duniani kote zaidi ya asilimia 70, wamewahi kupitia aina fulani ya ukatili wa kimwili tangu walipokuwa na umri wa miaka hiyo
Takwimu hizo za mwaka jana za shirika hilo zinaonyesha kuwa katika baadhi ya nchi, wasichana 7 kati ya 10 ambao ni waathiriwa wa ukatili wa kingono hawajawahi kuripoti vitendo hivyo, wengi wao wakidhani ni vitendo vya kawaida tu, na siyo ukatili.
Huku Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi ambazo watoto wa kike wanapitia vitendo hivyo Taswira ya habari imezungumza na baadhi ya wakazi jijini hapa ili kufahamu ni kwanini vitendo hivyo bado vipo katika jamii huku wakitaja suala la uoga hasa kwa wasichana wenyewe katika kuripoti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa likichangia.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo katika Mkoa wa Dodoma Bi Consolatha Michael anasema kuwa suala hilo linaanza katika ngazi ya familia endapo wazazi au walezi watakaa pamoja na kumuandaa mtoto kuwa mtu bora baadae katika familia yake watasaidia kupunguza matukio kama hayo ya ukatili.
Ripoti ya jeshi la polisi nchini inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 Huku watetezi wa masuala ya haki za watoto wakitaja imani za kishirikina na utandawazi kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa matukio hayo.