Nagulo Bahi wakabiliwa na changamoto ya kukosa Zahanati
13 April 2021, 12:35 pm
Na; Selemani Kodima
Licha ya mwongozo wa sera ya afya ya 2007 kuainisha kuwa kila Kijiji kitakuwa na Zahanati, hali ni tofauti katika Kijiji cha Nagulo Kata ya Bahi ambapo tangu kuanzishwa kwa Kijiji hicho hawajawahi kuwa na Zahanati.
Taswira ya Habari imezungumza na wakazi wazaliwa wa Kijiji hicho na kusema kuwa tangu kilipoanzishwa wamekuwa wakisafiri kwenda kutafuta huduma za afya katika vituo vya Afya vya Bahi au Kintiku.
Maria Emmanuel ni Mkazi wa Nagulo Bahi amesema zipo changamoto mbalimbali wanazopata kutokana na kukosekana kwa Zahanati ikiwemo huduma za kujifungua, na huduma za mama na mtoto.
Aidha baadhi ya wananchi wamesema jukumu ambalo wameendelea kulichukua ili kuweza kushiriki katika kutatua changamoto hiyo ni pamoja na kuchangia fedha kwa ajili ya hatua za mwanzoni lakini hali imebaki vilevile.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bahi Augustino Ndunu amekiri kuwepo kwa Changamoto hiyo na amesema katika mpango mkakati wanatarajia kuendelea kutatua tatizo la ukosefu wa Zahanati katika Vijiji vinavyopatikana ndani ya Kata yao.
Amesema zoezi la ujenzi wa Zahanati hizo umeanza katika Kijiji cha Uhelela kupitia msaada wa Shirika la Good Neighbors na baada ya hapo wataelekeza nguvu katika Kijiji cha Nagulo Bahi.
Kwa Mujibu wa sera ya afya ya mwaka 2007 Kila kijiji kitakuwa na zahanati. Kijiji chenye kituo cha afya, hakitakuwa na haja ya kuwa na zahanati. Huduma zitakazotolewa katika zahanati ni pamoja na; uboreshaji wa afya ,kinga, tiba na utengemao.