Wakulima wa mpunga Bahi wailalamikia tume ya umwagiliaji
31 October 2023, 11:21 am
Wakulima hao wanasema pamoja na kufuatilia kwa muda mrefu, bado tume ya umwagiliaji haijaonyesha ushirikiano katika kutatua kero hiyo.
Na. Bernad Magawa
Wakulima wa mpunga wilayani Bahi Wameilalamikia tume ya umwagiliaji kwa kushindwa kuwarekebishia miundombinu ya kilimo kwa miaka miwili sasa na kusababisha baadhi yao kukosa mavuno.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, mmoja wa wakulima hao ambaye pia ni kiongozi wa skimu ya Bahi sokoni Bwana Said Ibrahim amesema wamekuwa wakichangishwa michango na tume kwa ahadi ya kurekebishiwa miundombinu ya kilimo jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa hivyo kuiomba serikali iwasaidia.
Saidi amesema pamoja na kufuatilia kwa muda mrefu, bado tume ya umwagiliaji haijaonyesha ushirikiano katika kutatua kero hiyo huku akiweka wazi kiwango ambacho wakulima wameshangishwa mpaka sasa.
Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe akijibu ombi la wakulima hao ameahidi kulifanyia kazi kwa haraka ili wakulima waweze kuingia shambani katika msimu huu wa kilimo wakiwa na uhakika wa upatikanaji wa maji.