Wananchi watakiwa kutoa ushirikiano mradi wa uboreshaji milki za ardhi
7 September 2023, 2:51 pm
Chalinze ni miongoni mwa halmshauri 41 zinakazopitiwa na mradi wa Uboreshaji usalama wa milki za ardhi, ambapo Zaidi ya viwanja 7,600 vimepimwa, huku viwanja 50,000 vikitarajiwa kupimwa mpaka mwisho wa mradi huo.
Na Seleman Kodima.
Wakazi wa Chalinze wametakiwa kutoa ushirikiano kwa maafisa wanaotekeleza mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi nchini kwa kukubali kuchangia sehemu ya vipande vyao vya ardhi kwa lengo la kutenga maeneo maalum ya kijamii yatakayotumika kwa matumizi ya umma kama vile shule, huduma za afya, maeneo ya michezo pamoja na barabara.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo mhe. Halima Okash alipokua akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa mradi huo katika halmashauri ya Chalinze uliofanyika katika ukumbi wa Kikwete.
Aidha Mhe. Okash amesema kuwa ujio wa mradi huo utarahisisha upatikanaji wa miundombinu muhimu ya barabara ambayo imekua ni changamoto katika maeneo mengi ndani ya halmashauri hiyo jambo linalopelekea ukosefu wa huduma ya haraka pindi yanapotokea majanga ya moto, mafuriko au wagonjwa.