Madereva wanao fanya makosa kupewa adhabu
1 April 2021, 10:31 am
Na; Mariam Matundu.
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi George Simbachawene amesema wameweka utaratibu wa kutangaza majina ya madereva watakaokuwa wanafanya makosa ya kujirudia kila mwezi ikiwa ni sambamba na adhabu mbalimbali.
Mh.Simbachawene ameyasema hayo hii leo na kutangaza kuwafungia madereva 10 leseni zao walio fanya makosa ikiwemo mwendo kasi kwa kipindi cha mwezi Septemba 2020 hadi Machi 2021 kwa miezi mitatu.
Pamoja na adhabu hiyo waziri Simbachawene ameagiza madereva hao wapewe mtihani wa udereva na ambao hawatafaulu wafutiwe leseni zao moja kwa moja.
Aidha amemuagiza mkurugenzi wa LATRA kuwasilisha taarifa za madereva wote waliobainika kukiuka matumizi ya vidhibiti mwendo VTS kila mwezi katika ofisi ya waziri wa mambo ya ndani ya nchi.
Pamoja na hayo ameliagiza jeshi la Polisi kuhakikisha wanafanya ukaguzi ipasavyo kwenye magari na iwapo gari halina sifa za kusafiri wahakikishe wanazuia safari kwa gari hilo.
Hatua hii ina lengo la kuhakikisha ajali zinazogharimu maisha ya watanzani zinadhibitiwa ambapo hivi karibuni imetokea ajali kubwa eneo la babati kilomita 5 (tano) kutoka kituo cha Makatani iliyosababisha vifo vya watu nane na majeruhi zaidi ya 50.