UMISETA wahimizwa nidhamu
7 June 2023, 4:19 pm
Afisa usalama wilaya ya Kongwa Bwana Mwakasendo amesisitiza kuzingatia muda na kuwa wavumilivu kuendana na ulimwengu tulionao kwani muda ni siri ya ushindi.
Na Bernadetha Mwakilabi.
Wanafunzi 115 wa shule za sekondari wilayani Kongwa wanaoshiriki mashindano ya umoja wa michezo kwa sekondari UMISETA wametakiwa kudumisha heshima, nidhamu na kuzingatia mambo ya msingi waliyoelekezwa na walimu wao wa michezo.
Hayo yameelezwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kongwa Dkt. Omary Nkullo alipokuwa akiwaaga wanafunzi hao kuelekea kwenye mashindano ya UMISETA mkoani Dodoma ambapo amesema kuwa anatarajia ushindi kutoka kwao.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel ameunga mkono suala la nidhamu na kuongeza kuwa anathamini umuhimu wa michezo kwani ni chanzo cha ajira na afya njema.
Aidha Mwema amewataka wanafunzi hao kumtegemea Mungu katika mazoezi na mashindano hayo ili waweze kufanikiwa zaidi.