Wakazi kata Ntyuka kuondokana na adha ya maji
2 June 2023, 1:21 pm
Na Selemani Kodima.
Wakazi 4,441 wa mitaa ya Chimalaa na Nyerere kata ya Ntyuka jijini Dodoma wanatarajiwa kuondokana na adha ya kutopata uhakika wa maji safi na salama baada ya uzinduzi wa mradi wa maji wa Ntyuka Chimalaa kukamilika .
Wakizungumza katika uzinduzi wa mradi huo ambao umetekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA ), baadhi ya wananchi wa kata hiyo wameeleza furaha yao baada ya uzinduzi huo na namna walivyoteseka miaka ya nyuma kutafuta huduma ya maji safi na salama
Katika tukio hilo la uzinduzi wa mradi wa maji ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema uzinduzi wa mradi huo ni hatua kubwa ambayo itasaidia kubadilisha mifumo ya maisha kwa wanajamii wa Ntyuka.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph, amesema kuwa mradi huo utawanufaisha wakazi zaidi ya 4,441 katika maeneo ya Ntyuka mtaa wa Chimalaa na Nyerere ambao kwa sasa watapata maji kwa asilimia 97 kutoka asilimia 0 ya awali.
Naye diwani wa kata ya Ntyuka Yona Andrea amesema kuwa mradi huo wa maji utawanufaisha wakazi wapatao 13,543 ndani ya kata yake huku akimwomba Waziri wa Maji kuwasaidia kupeleka huduma ya maji kwenye zahanati ya Ntyuka .
Imeelezwa kuwa gharama kamili za kutekeleza mradi huo wa maji wa Ntyuka Chimalaa ni kiasi cha shilingi milion 471.8 ikiwa ni hatua muhimu ya utatuzi wa adha ya maji kwa wakazi wa jiji la Dodoma.