Dodoma FM

Waziri Ummy awataka Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuendelea kuchapa kazi

5 May 2021, 10:13 am

Na; Nteghenjwa Hosseah

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa Mhe.Ummy Mwalimu amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kuchapa kazi kama awali na sio kukaa kusubiria uteuzi.

Waziri Ummy ameyasema hayo katika ziara yake Wilayani Chemba Mkoani Dodoma kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na Kamati ya Fedha pamoja na Menejimenti ya Halmashauri hiyo tarehe 04.05.2021.

“Hali inayoendelea kwa viongozi hawa haileti Afya, wengine hawafanyi kazi eti wanasubiria mkeka, hamuoni kuwa mnaonea wananchi kupata haki yao ya msingi ya kuhudumiwa” alihoji Waziri Ummy.

Kipindi hiki mnatakiwa kuendelea kuchapa kazi kama kawaida kwani wananchi wanahitaji kuendelea kuhudumiwa, suala la mkeka unakuja lini hilo ni kuliacha Mamlaka, ninyi chapeni kazi” aliongeza Mhe. Ummy

Aidha Mhe. Ummy aliwakumbusha viongozi hao kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi huku wakimtanguliza Mungu mbele ambaye ni mpangaji wa kila jambo.