Dodoma FM

Wakazi wa Nzuguni waiomba Serikali iwaboreshee barabara

26 January 2022, 4:16 pm

Na; Neema Shirima.

Baadhi ya wananchi katika Kata ya Nzuguni  jijini Dodoma wameiomba Serikali iwaboreshee miundombinu ya barabara pamoja na daraja katika mto unaotenganisha Nzuguni A na B ambapo umekuwa changamoto wakati wa mvua.

Wakizungumza na Taswira ya habari wananchi hao wamesema katika msimu wa mvua wanashindwa kupita hali inayokwamisha shughuli za kimaendeleo.

Taswira ya habari imemtafuta Diwani wa Kata ya Nzuguni Bw.Aloyce Luwega na amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo amesema tayari ujenzi wa daraja hilo umeshaanza lakini kutokana na mvua zinazoendelea ujenzi umesimama.

Aidha amewaomba wananchi wake kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki cha ujenzi wa daraja ambapo litakamilika hivi karibuni ili kurahisisha shughuli za kijamii.

Baada ya kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Kata ya Nzuguni hatimaye Serikali imesikia kilio hicho na tayari ujenzi wa barabara na daraja umeanza.

Usipoziba ufa utajenga ukuta ambapo ujenzi wa barabara na daraja hilo umeanza mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa zaidi ambapo hatimaye siku si nyingi wananchi wataanza kunufaika na ujenzi wa miundombinu hiyo.