Dodoma FM

Wananchi watakiwa kupata elimu sahihi juu ya chanjo ya uviko 19

5 October 2021, 11:19 am

Na; Shani Nicolous.

Kufuatia zoezi la kuendelea kujikinga na Uviko 19 Dodoma imeonekana kuwa na mwitikio mkubwa katika suala la uchanjaji.

Akizungumza na Taswira ya habari Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Jabir Shekimweli amesema kuwa kuna mwitikio mkubwa wa kuchanja kwani Dodoma mjini zilikuwepo chanjo elfukumi na tano na tayari chanjo elfukumi na mbili zimetolewa kwa watu.

Amesema kuwa ni jukumu la kila mtu kupata elimu sahihi bila kukimbilia mitandao ya kijamii yenye elimu ya upotoshaji juu ya chanjo ya Uviko 19 ,hivyo ikiwa mtu hana uelewa sahihi juu ya chanjo hiyo ni bora kutafuta njia bora ya kuelimishwa na si kupotosha.

Kwa upande wake mganga mkuu wa Wilaya Andrew Methew amesema kuwa watu waache wasiwasi na mashaka juu ya chanjo ya Uviko 19 kwa kuwa serikali imethibitisha ubora na usalama wake na hakuna aliyepata athari zozote baada ya kupata chanjo hiyo.

Baadhi ya walimu kutoka shule tofauti jijini hapa wamethibitisha kupata chanjo hiyo na kutokupata madhara yoyote , wamewashauri wananchi kuchanja kwa manufaa ya afya zao na jamii kiujumla.

Kupitia mpango wa utoaji elimu kwa watumishi wa umma na wananchi wote Mkuu wa wilaya Dodoma mjini mapema wiki hii amefanya mazungumzo na walimu wa shule za msingi na sekondari yaliyojumuisha elimu juu ya chanjo ya Uviko 19