Dodoma FM

Ukosefu wa miundombinu rafiki katika shule jumuishi watajwa kuwa changamoto kwa watu wenye ulemavu

1 October 2021, 12:40 pm

Na; Shani Nicolous.

Ukosefu wa miundombinu rafiki yakujifunzia katika shule jumuishi nchini imetajwa kuwa changamoto hivyo kuathiri maendeleo ya watu wenye ulemavu.

Akizungumza na Taswira ya habari mkurugenzi mtendaji wa kituo cha habari kuhusu walemavu ICD Fredrick Mkatambo amesema kuwa mfumo wa elimu maalaumu unachangamoto nyingi ndiyo maana jamii imetakiwa kufahamu umuhimu wa mfumo wa elimu jumuishi pamoja na kwamba miundombinu ni changamoto kwao.

Amesema kuwa mfumo wa elimu maalumu unaweza kuchangia baadhi ya watoto kukosa haki za msingi kutokana na umri lakini pia kupoteza asili na tamaduni zao kwa kusoma mbali na nyumbani kutokana na wazazi wengi kuwapeleka watoto shule maalumu na kuwatelekeza watoto huko.

Ameongeza kuwa watoto wenye mahitaji maalumu kuchanganyikana na wengine inatengeneza umoja na kuondoa unyanyapaa kwa kuwa tayari wamezoeana na kupendana pamoja na kupewa ushirikiano kutoka kwa wenzao.

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa elimu jumuishi kutoka FPCT Jane Mgidange amesema kuwa wameweza kutengeneza baadhi ya mazingira rafiki kwa baadhi ya shule ambazo zilikuwa ni changamoto kwa wanafunzi wa mahitaji maalumu katika shule jumuishi kwa kutoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi kiujumla.

Msingi wa mafunzo mbalimbali katika jamii ni chachu ya kuondoa mawazo mgando juu ya watu wenye mahitaji maalumu kuwa hawawezi, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kutoa ushirikiano hitajika kwa watu wenye mahitaji maalumu hasa katika upande wa elimu.