Dodoma FM

Waziri Ummy apiga marufuku walimu kuhama kabla ya kupeleka walimu wengine

9 September 2021, 1:20 pm

Na;Mindi Joseph .

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali Mhe Ummy Mwalimu amepiga marufuku kuhamisha walimu kutoka katika Halmashauri zilizoko pembezoni Nchini kabla ya kupeleka walimu mbadala.

Akifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi Tawi la Tume ya Utumishi wa Walimu leo Jijini Dodoma Waziri Ummy amesema kuwa ni marufuku kuhamisha walimu kutoka katika Halmashauri zilizoko pembezoni kabla ya kupeleka waalimu mbadala na ameitaka tume ya utumishi wa walimu nchini kuhakikisha kabla ya kuwahamisha walimu inapeleka waalimu mbadala.

Ameongeza kuwa walimu wanaotaka kuhama kutoka mijini kwenda vijijini ni ruksa kwani uhamisho ni haki ya mtumishi lakini changamoto kubwa wengi wanataka kuhama kutoka Halmashauri za vijijini kwenda mijini wakati haiwezekani .

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imejikita katika kutoa elimu bora kwa jamii kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora ya kufundisha na kujifunzia ni wajibu wa tume sasa kuhakikisha uwiano wa walimu unafanyika ili kutoa elimu sawa kwa watoto wote wa Kitanzania hasa katika Halmashauri zilizopo pembezoni.

Aidha ameitaka tume ya Utumishi wa Walimu kufanya tathmini ya kina kwa kuangalia uwiano wa waalimu kwenye shule za Msingi na Sekondari katika Mamlaka za Serikali za Mitaa lengo likiwa ni kuwa na takwimu sahihi za mahitaji halisi ya walimu na uwiano uliosawa katika Halmashauri.