Dodoma FM

Fedha za makato mbalimbali zatarajia kujenga madarasa zaidi ya 500 kwa shule za msingi na sekondari nchi nzima.

2 September 2021, 2:24 pm

Chanzo: Dawati

Rais wa Jamhuri yamuungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inatarajia kujenga madarasa zaidi ya 500 kwa shule za msingi na sekondari Nchi nzima kupitia makato katika tozo mbalimbali.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa jimbo la Kawe Mkoani Dar es salaam akiwa safarini kuelekea Bagamoyo Mkoani Pwani katika mwendelezo wa zoezi la kurekodi kipindi maalumu cha The Royal Tour kinacholenga kuutangaza utalii na fursa zilizopo Nchini.

Amesema pamoja na Serikali kusikia kilio cha wananchi juu ya gharama kubwa za tozo katika miamala ya simu na hatimae kushushwa kwa gharama hizo kwa asilimia 30 hivyo fedha zitakazokuwa zikikusanywa katika awamu hii zitaelekezwa moja kwa moja katika ujenzi wa madarsa zaidi ya 500 Nchini.

Aidha Rais Samia amesema Serikali yake itahakikisha inakamilisha miradi yote iliyoanzishwa na aliekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dk. John Pombe Magufuli ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mipya.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Amos Makala amesema amenzisha utaratibu wa kupita jimbo kwa jimbo ili kuona maendeleo ya wananchi huku Mbunge jimbo la Kawe Askofu Josephat Gwajima akimuomba Rais Samia kuwajengea shule ya msingi na asekondari katika Mtaa wa Kunduchi.