Dodoma FM

Serikali kuendeleza maboresho sera ya matibabu bure kwa wazee

25 June 2021, 1:24 pm

Na;Yussuph Hans.

Serikali imesema katika kuhakikisha wazee wanapata huduma bora ya matibabu, inaendeleza zoezi la utambuzi na kuwapatia vitambulisho ambapo mpaka kufikia Machi 2020/2021 Asimilia 87 ya makadirio ya Wazee wote nchini wamepatiwa Vitambulisho hivyo.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Godwin Molel wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini Mh.Shamsia Azizi Mtamba aliyehoji ni lini Serikali itawapatia bima ya afya wazee hasa maeneo ya Vijijini.

Dkt.Molel amesema kuwa huduma za tiba ni haki ya msingi kwa wazee wote, hivyo Serikali inaimarisha upatikanaji wa huduma hizo ikiwemo uwepo wa dirisha maalumu kwa ajili ya matibabu yao na kupatiwa bima za afya.

Ameongeza kuwa takribani asilimia 87 ya makadirio ya wazee nchini wamefikiwa na Huduma ya Bima ya Afya, kati yao wakiwemo Wanawake na Wanaume pamoja na Wazee wasiojiweza.

Aidha Serikali inafanya kazi katika la kudhibiti dawa ili kuhakikisha kila kituo cha afya kinakuwa na dawa za kustosha.

Mikakati mbalimbali imekuwa ikiwekwa na Serikali ili kuhakikisha wazee wanapata huduma bora za afya na mwaka uliopita ilianzisha zoezi la kuwatambua na kuwapatia vitambulisho.