Dodoma FM

Serikali kuandaa mikakati mbalimbali ili kupambana na biashara ya dawa za kulevya

2 June 2021, 11:12 am

Na;Yussuph Hans.

Serikali imesema haitofumbia macho suala la baadhi ya viongozi wanaofichua siri na mipango ya Serikali katika udhibiti wa Dawa za kulevya Nchini.

Hayo yamebainishwa Bungeni na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na wenye ulemavu Mh.Jenista Mhagama wakati akijibu swali la Mbunge wa Malindi Mh.Mohammed Omar aliyehoji hatua gani zimefikiwa na serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika kipindi cha mwaka 2019/2020.

Mh.Mhagama amesema kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa katika kudhibiti dawa za kulevya huku kukiwa na changamoto kwa baadhi ya maafisa wa vyombo mbalimbali kufichua siri katika udhibiti wa biashara hiyo.

Ameongeza kuwa katika kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya Serikali imetekeleza mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya dawa hizo.

Aidha katika kipindi cha mwaka 2019/2020 imetambua mitandao mikubwa ya wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya, kubaini mianya ya uingizaji na kuidhibiti kwa kiasi kikubwa.

Bunge limeendelea leo jijini Dodoma ambapo wizara ya nishati na madini imewasilisha bajeti yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.