Dodoma FM

TAWOMA watakiwa kujenga masoko mapya ya madini

5 December 2020, 11:53 am

Na Alfred Bulahya,

Dodoma.

Serikali imekitaka Chama Cha wachimba Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) kuendelea na juhudi za kujenga masoko mapya ya Madini ili kuhamasisha upatikanaji wa soko la Madini hasa Yale yasiyo na thamani.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na Kamishina wa Madini Nchini Injinia David Mulabwa wakati akizindua Duka jipya la kuuzia bidhaa zinazotokana na Madini la Chama Cha Wanawake wachimba Madini Tanzania (TAWOMA)
Aidha amesema kuwa Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuwaendeleza wachimbaji nchini ikiwemo kuwapa mafunzo mbalimbali kupitia mikutano ili kuimarisha shughuli zao na hivyo kuamua kuongea na Benki ili waweze kukopesheka.

Katika hatua nyingine Kamishina huyo amesema kuwa tayari Serikali ilishaondoa Kodi kwenye vifaa vya uongezaji thamani wa Madini, hali iliyorahisisha upatikanaji wake.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kufanya mazungumzo na Uongozi wa Benki mbalimbali nchini ili kuhakikisha Wachimbaji hao wanakopeshwa vifaa vya uchimbaji kwa lengo la kuimarisha shuguli zao.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Wachimba Madini Wanawake( TAWOMA) Salma Kundi amesema mikakati yao ni kahakikisha wanaondoa umaskini kwa wanawake huku akieleza changamoto zilizopo .
Ametoa wito kwa Wanawake kujiunga Katika Chama hicho ili kujiongezea kipato Chao na Taifa kwa ujumla kwani uchimbaji wa Madini ni moja ya ajira inayopatikana nchini.
Baadhi ya wachimbaji wanawake waliohudhuria katika uzinduzi huo wamesema TAWOMA imeleta mapinduzi kwenye sekta ya madini ikiwemo kukomesha unyanyasaji na ukatili kwa wachimbaji wanawake.