Dodoma FM

Wataalam wa mipango, uratibu watakiwa kutenga bajeti kutekeleza program ya MMMAM

2 June 2023, 6:45 pm

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum  Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya utekelezaji wa Programu hiyo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii. Picha na Mariam Matundu.

Waziri Dkt. Gwajima amesema katika bajeti zijazo itabidi uhakiki wa bajeti ufanyike ili kubaini kama bajeti ya utekelezaji wa Programu hiyo umezingatiwa.

Na Mariam Matundu.

Rai imetolewa kwa wataalam wa mipango na uratibu katika sekretarieti za mikoa kuhakikisha wanatenga bajeti za utekelezaji wa programu jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) ili kufanikisha malengo ya uanzishwaji wa programu hiyo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum  Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya utekelezaji wa programu hiyo kwa maafisa maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii, makatibu tawala wasaidizi wa mipango na uratibu wa sekretarieti za mikoa na wadau jijini Dodoma Juni 1, 2023.

Sauti ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa jitihada za wizara na wadau kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa programu hiyo.

Sauti ya Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii.
Washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza hotuba iliyotolewa na viongozi hao. Picha Mariam Matundu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Children in Crossfire, Craig Ferla amesema mara nyingi kuna changamoto ya utekelezaji wa programu hasa ngazi za chini hivyo ni faraja ya pekee kuwa na makatibu tawala wasaidizi wa mipango na uratibu kwenye mafunzo haya.

Sauti ya Mkurugenzi wa Shirika la Children in Crossfire.

Naye Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Mkoa wa Dar es Salaam Chillah Moses ameishukuru Wizara kwa jitihada zinazofanywa kuhakikisha utengaji wa bajeti ya kutekeleza programu hiyo kwa manufaa ya watoto nchini.