Dodoma FM

Kongwa: Wananchi waridhia kuhama kupisha chanzo cha maji

29 May 2023, 7:39 pm

Ziara ya ukaguzi wa chanzo cha maji kilichopo kitongoji cha Kawawa Kibaigwa wilayani Kongwa. Picha Bernadetha Mwakilabi.

Na Bernadetha Mwakilabi.

Wananchi wa kitongoji cha Kawawa kilichopo katika mamlaka ya mji mdogo Kibaigwa wilayani Kongwa wameridhia kuhama ili kupisha eneo la chanzo cha maji lililopo kitongojini hapo lenye ukubwa wa hekari 28.

Hayo yamejiri mapema katika ziara yake mkuu wa wilaya Kongwa ambapo wananchi hao wamesema kuwa wapo tayari kuhama katika eneo hilo endapo watapatiwa fidia ya maeneo mengine ya kuishi kwani suala la maji ni muhimu kwao na jamii nyingine inayowazunguka kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya taifa. Akiongea kwa niaba ya wananchi hao Bwana Abineli Maine anasema

Sauti ya Bw. Abinel Maine.

Akitolea ufafanuzi wa mgogoro wa eneo hilo meneja wa mamlaka ya maji safi DUWASA mamlaka ya mji mdogo Kibaigwa Bwana Emmanuel Mhando Amesema kuwa eneo hilo kwa sasa ni la Mamlaka ya Maji Safi DUWASA na lilikabidhiwa kwao kabla ya mwaka 2018  na kutengwa kuwa eneo tengefu kwa ajili ya chanzo cha maji linaloweza kulisha eneo la mamlaka ya mji mdogo Kibaigwa, mkoa wa Dodoma na mikoa mingine ya jirani.

Sauti ya Meneja wa mamlaka ya maji safi DUWASA mamlaka ya mji mdogo Kibaigwa
Ziara ya ukaguzi wa chanzo cha maji kilichopo kitongoji cha Kawawa Kibaigwa wilayani Kongwa. Picha Bernadetha Mwakilabi.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel amewaagiza wataalam wakiwemo wanasheria na DUWASA kufuatilia kwa haraka kiundani na kujiridhisha kupata taarifa sahihi juu ya idadi ya watu wanaostahili kupewa fidia ya eneo hilo pasipo kumdhulumu mtu yeyote.

Sauti ya mkuu wa wilaya Kongwa .

Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa Bwana Samwel Mganga amewashukuru wananchi wa Kawawa Kwa hatua hiyo ya kuridhia kuachia eneo hilo kuwa wameonesha ukomavu wa fikra na kuona umuhimu wa maji katika maisha yao.

Sauti ya mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa