Dodoma FM

Mitandao yachangia ukatili wa kijinsia kwa vijana balehe

10 March 2023, 3:39 pm

Profesa wa Hisabati ,Prof. Verdiana Masanja akiwa pamoja na Mkurugenzi wa TGNP, Bi.Lilian Liundi na wadau wengine wakimsikiliza mmoja wa wabunifu wanawake wakionesha ubunifu wao katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo Machi 9,2023 yanayoendelea kwa siku mbili katika Viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Jijini Dar es salaam. picha na sayari news.

Profesa huyo ameiomba serikali kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo huku akipendekeza kutungwa kwa kanuni zenye mlengo wa kijinsia zitakazotoa ulinzi maalum kwa watoto wa kike na wanawake dhidi ya ukatili wa mtandaoni.

Na Zania Miraji.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 4 ya watumiaji wa mitandao walio na umri kati ya miaka 12 hadi 17 wanapitia changamoto ya ukatili wa kijinsia kwenye mitandao.

Takwimu hizo zimetolewa na Profesa wa Hisabati Verdiana Masanja tarehe 9 Machi 2023  katika siku ya maadhimisho ya wanawake iliyoandaliwa na mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam.

Profesa Verdiana akiwa ni mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ameeleza kuwa walio wengi hufanyiwa ukatili katika mitandao ya kijamii pamoja na kwamba serikali imetunga sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi kuhakikisha kila mtu anakuwa salama anapotumia vifaa vya teknolojia.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi TGNP Bi. Gemma Akilimali ameeleza kuwa taarifa ya UN Women Gender Snapshots ya mwaka 2022 inaonesha kuwa wanawake wengi hawapo katika ulimwengu wa kidigitali hali inayopelekea kupoteza dola za kimarekani trilioni 1 katika pato la Taifa kwa nchi zenye uchumi wa chini na wa kati.

Kauli mbiu mwaka huu inasema Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia chachu kuleta usawa wa kijinsia.