Dodoma FM

UWT yaweka wazi wanawake wanavyo ogopa kuwania nafasi za uongozi

8 March 2023, 5:01 pm

Umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT).Picha na Benard Magawa.

Wanawake wa kata ya Bahi wilayani Bahi wamezungumzia ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Na Benard Magawa.

Katika kusherehekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambayo hufanyika machi 8 ya kila mwaka, wanawake wa kata ya Bahi wilayani Bahi wamezungumzia ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT) kata ya Bahi Mgeni Juma wakati akizungumza na kituo hiki na kueleza namna wanawake wanavyo ogopa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa sababu ya uoga.

Idadi ya Viongozi wanawake katika kata ya Bahi bado ni ndogo sana kwani wengi wamekuwa na uoga katika kuthubutu

“Idadi ya Viongozi wanawake katika kata ya Bahi bado ni ndogo sana kwani wengi wamekuwa na uoga katika kuthubutu huku wengine wakiona aibu kushiriki masuala ya uongozi kwa kuwahofia waume zao.” Amesema Mgeni.

Sauti ya mgeni Juma.

Naye katibu wa Uwt kata ya Bahi Neema Iwinga amesema pamoja na wanawake wengi kutokushiriki vizuri katika uongozi bado wao wamekuwa nguzo katika malezi kuhakikisha watoto wanakuwa na maadili mazuri katika jamii.

Amesema kwa sasa kuna changamoto kubwa ya mporomoko wa maadili katika jamii lakini wanawake bado wapo mstari wa mbele kuhakikisha malezi ya watoto na vijana hayatetereki ili kuwa na kizazi chenye nidhamu na hofu ya Mungu.

Sauti ya katibu wa Uwt kata ya Bahi Neema Iwinga.

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Bahi Sokoni Magreth John anaeleza changamoto wanazokutana nazo kama wanawake wakati wa kuomba nafasi mbalimbali za uongozi kupitia uchaguzi.

“Wanawake tunakutana na changamoto nyingi sana wakati wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, lakini niwasihi wanawake wenzangu msiogope hata sisi tunao uwezo mkubwa wa kuwa viongozi katika jamii tunazoishi.” Amesema Magreth.

Sauti ya Mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Bahi Sokoni Magreth.

Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kwa mwaka 2023 yamefanyika kimkoa wilayani kondoa yakiongozwa na kauli mbiu isemayo Ubunifu na Mabadiliko ya taknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia.