Dodoma FM

Adaiwa fedha watoto wafutwe shule

15 February 2023, 10:41 am

Wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Raisi Dkt. Samia Suluhu Hasani ikiendelea kuboresha miundombinu ya elimu ili kila mtoto wa kitanzania apate elimu ya Msingi.Picha na daily news

Na Benard Magawa.

Wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Raisi Dkt. Samia Suluhu Hasani ikiendelea kuboresha miundombinu ya elimu ili kila mtoto wa kitanzania apate elimu ya Msingi na Sekondari bila malipo ili kutokomeza kabisa uwepo wa adui UJINGA katika taifa hili, familia ya Bw. Andrea Nkombii wa kijiji cha Uhelela Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma amewalalamikia baadhi ya walimu kijijini hapo kudai fedha ili kuwaondoa shuleni watoto wao.

Akizungumza kwa masikitiko Mama wa familia hiyo Telezia Mikaeli amesema.

“wamefuatwa na walimu mara kadhaa wakidai fedha shilingi elfu 40 ili wamfute mtoto wao Bonifasi Andrea ambaye alipaswa kuwa darasa la saba mwaka huu wakidai kuwa anapata ufaulu mdogo darasani, huku wakidai kiasi cha shilingi elfu 60 ili kumfuta binti yao Emilia Andrea ambaye wanadai hajui kusoma vizuri.”

Mama huyo ameyasema hayo February 14,2023 nyumbani kwao kijiji cha uhelela na kueleza kuwa walimu hao (Majina yamehifadhiwa) wamekuwa na tabia ya kuwadai fedha baadhi ya wazazi kijijini hapo ili wawafute watoto wao shule kitendo ambacho amekiita ni ukatili kwa kuwanyima watoto haki ya msingi ya kupata elimu huku akiomba msaada ili watoto wao waendelee na masomo.

Telezia Mikael.

“Sisi wazazi hatukufanikiwa kusoma vizuri, tunategemea watoto wetu wasome ili watusaidie katika mambo mengi lakini sasa kwanini hawa walimu walioletwa kutuelimisha tena wawe chanzo cha watoto wetu kuacha shule?.” Alihoji Telezia.

Walipohojiwa watoto, Boniface Andrea alikiri kufutwa shule kwa kupata ufaulu mdogo huku akiweka wazi kiwango cha alama alizokuwa akipata wakati mtoto Emilia Andrea ambaye inasemekana alipaswa kuwa darasa la nne mwaka huu akisema aliacha kwenda shule baada ya kurudishwa darasa.

Boniface Andrea.
Emilia Andrea.

Naye Diwani wa kata ya Bahi Mhe. Agostino Ndonuu ambaye ndiye muwakilishi wa wananchi katika kata hiyo amesema jambo hilo halikubaliki na linarudisha nyuma juhudi za serikali katika sekta ya elimu na kuahidi kulifuatilia kwa kina ili sheria ichukue mkondo wake kwa wote watakao bainika kuhusika na jambo hilo.

Diwani wa kata ya Bahi Mhe. Agostino.

Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ndiyo Halmashauri Pekee iliyoingia nafasi kumi bora kitaifa kwa kushika nafasi ya kumi kwa nchi nzima ikitanguliwa na Majiji na Manispaa kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2022 huku ikiendelea kuwa kinara mkoani Dodoma kwa miaka mitatu mfululizo.