Dodoma FM

Wakazi wa Nzinje waiomba DUWASA kuwatatulia kero ya maji

16 December 2021, 2:22 pm

Na;Mindi joseph .

Wakazi wa mtaa wa Nzinje jijini Dodoma wameiomba Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira DUWASA kuwasaidia kutatua changamoto ya maji inayowakabili kwa muda mrefu.

Wakizungumza na Dodoma Fm baadhi ya wananchi hao wanasema kutokana na changamoto hiyo imewalazimu kutumia maji ya kwenye korongo na visima vya kuchimba ambayo si safi na salama hali inayohatarisha afya zao.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nzinje Bw.Godfrey Samweli amesema DUWASA waliwaahidi wananchi hao kuwapatia maji ya bomba lakini hadi sasa hawajatimiziwa ahadi hiyo.

Kwa upande wake Mhandisi Oresti John kutoka DUWASA amesema eneo hilo lipo kwenye mpango wa maboresho ya kupata maji na tayari mamlaka hiyo imeshatengeneza uchimbaji wa kisima chenye uwezo wa kuzalisha lita elfu 8 kwa saa.

Mtaa wa Nzinje unakadiriwa kuwa na wakazi elfu 1050 na hadi sasa bado wanatumia maji ya kuchota kwenye visima vya maji ya chemchem.