Dodoma FM

Ukarabati wa barabara katika kata ya Dabalo utachangia kukua kwa maendeleo

12 August 2021, 11:27 am

Na; Benard Filbert.

Kufuatia Kukamilika kwa ukarabati wa barabara za ndani ya kata ya Dabalo wilayani Chamwino itasaidia kukua kwa maendeleo ya wakazi wa kata hiyo.

Hayo yameelezwa na Diwani wa kata hiyo bwana Isihaka Rajabu wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu mkakati wa serikali ya kata kufanya marekebisho ya barabara korofi.

Amesema mpaka hivi sasa tayari wamefanikiwa kurekebisha barabara nyingi zilizopo katika kata ya Dabaro kwa kushirikiana na TARURA ikiwepo kuelekea katika machimbo ya madini katika kijiji cha nali.

Kadhalika amesema kutakuwa na mzunguko mkubwa wa biashara kwani hakuna shida ya barabara hivyo watakuwa wanasafirisha madini hadi Dodoma mjini.

Amewataka baadhi ya wananchi kutunza miundombinu hiyo na kuepusha kupitisha mifugo kwani inaweza kuharibu barabara.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Dabalo wamesema kukamilika kwa ukarabati wa baadhi ya barabara katika kata hiyo kutachagiza maendeleo ikiwepo kusfirisha mazao pasipo usumbufu kama awali.

Kukamilika kwa ujenzi wa barabara katika kata ya Dabalo itasaidia kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja katika eneo hilo kutokana na kuwepo kwa machimbo ya madini katika kijiji cha nali.