Dodoma FM

Kamati ya kudumu ya bunge yaridhishwa na utekelezwaji wa miradi Dodoma

5 May 2021, 10:41 am

Na; Mindi Joseph

Kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo,Mifugo na Maji imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji Mzakwe jijini Dodoma  na Buigiri Wilayani Chamwino inayotajwa kupunguza adha ya maji kwa wananchi.

Akizungumza   katika ziara hiyo,Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya kilimo,Mifugo na Maji Christina Ishengoma ameipongeza  Wizara ya Maji kwa kuendelea kutekeleza miradi hiyo kwa ufasaha itakayosaidia kutatua tatizo la maji Dodoma.

Naye  Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema takriban visima 10 vimechimbwa katika jiji la Dodoma na mpango  mkakati uliopo sasa ni utekekelezaji wa mradi wa maji kutoka ziwa Victoria.

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira jijini Dodoma Mhandisi Aron Joseph amesema mradi wa maji Buigiri Chamwino uliokuwa na thamani ya shilingi bilioni 2.5  umegharimu shilingi milioni 998 na hadi sasa umefikia asilimia 98.

Aidha  Kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo,Mifugo na Maji imeishauri Wizara pamoja na taasisi zake ikiwemo mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jiji la Dodoma [DUWASA] kuwa na mpango kabambe wa kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujenga nyumba zenye miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kwa wingi ili kuondoa changamoto ya uhaba wa maji.