Dodoma FM

Serikali yakiri hakuna malimbikizi ya malipo ya Pensheni kwa wastaafu

23 April 2021, 9:14 am

Na; Yussuph Hans

Serikali imesema imelipa mafao mbalimbali kwa Wanachama waliokidhi vigezo ambapo katika kipindi cha Julai Mwaka 2020 mpaka Mwezi Machi Mwaka huu, imewalipa jumla ya Watumishi 93,661 Mafao yenye thamani ya Tsh Bilioni Mia Tatu Sabini na Saba na Milioni Mia Nane.

Hayo yamejiri leo Bungeni Jijini Dodoma, wakati Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira  Mh. Patrobas Katambi alipokuwa akijibu swali la msingi la Mh Amina Daudi Hassani Mbunge wa Viti Maalum lililohoji ni Lini serikali itaondoa tatizo la ucheleweshwaji wa mafao kwa wanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF.

Mh katambi amesema kuwa Serikali imekuwa ikihakikisha wastaafu wote wanalipwa mafao kwa mujibu wa sharia  ambapo kwa mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF hutoa mafao kwa wanachama waliokidhi vigezo ndani ya siku 30.

Aidha amesema kuwa malipo ya mafao ya pensheni kwa wastaafu hulipwa kila mwezi ifikapo tarehe 25 katika akaunti ya wastaafu na mpaka sasa hakuna malimbikizo ya mafao ya pensheni kwa wastaafu.

Akijubu swali la nyongeza la Mbunge huyo lililohoji kwanini wastaafu wanachukua muda mrefu katika kufatilia mafao yao, Mh katambi amesema  mkakati wa serikali kwa sasa ni kuchunguza madai pamoja na tathmini ya madai endapo mfuko utajiridhisha utalipa madeni hayo.