Dodoma FM

Wafanyabiashara wahimizwa kulipa kodi bila shurti

2 April 2021, 12:46 pm

Na; Shani Nicolous

Wito umetolewa kwa wafanyabiashara nchini kulipa kodi bila kushurutishwa ili kukuza uchumi wa nchi.

Ushauri huo umetolewa ikiwa ni siku moja baada ya agizo alilotoa rais Mh.Samia Suluhu Hassan juu ya kutumiwa kwa njia sahihi za sahihi na rafiki katika ukusanya kodi kwa wafanyabiashara nchini.

Dodoma Fm imezungumza na mchumi Bw. Frank Micker ambapo amesema kuwa maagizo ya Rais Mh.Samia Suluhu ni hatua njema kwani itawafanya wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiyari bila kusukumwa na kuacha kufunga kwa hofu ya kuchukuliwa hatua kali.

Amesema kuwa mazingira wezeshi kibiashara yatawafanya watu kuanzisha biashara nyingi tofauti na hapo awali ambapo watu walikuwa na hofu huku wengine wakifunga biashara zao, huku pia akiwashauri wafanyabiashara kutambua wajibu wao kwa kulipa kodi bila usumbufu.

Kwa upande wao wafanyabiashara jijini Dodoma wamesema kuwa kauli ya Rais Mh.Samia Suluhu imewatia moyo na kuwapa hamasa ya kufanya biashara ambapo wameiomba Serikali kutengeneza utaratibu mzuri wa ukusanyaji kodi utakaoepusha kuyumba kwa biashara zao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha Mawaziri aliowateua  alimtaka waziri wa fedha kutumia njia sahihi za ukusanyaji wa kodi.