Dodoma FM

Simanzi na Vilio vyatanda jijini Dar es salaam

20 March 2021, 10:11 am

Na, Mariam Kasawa.

Maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na viongozi wastaafu wa Serikali zilizopita wamefika Uwanja wa Uhuru kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk.John Magufuli.

Maelfu ya wananchi walianza kujitokeza Uwanjani hapo mapema alfajiri ya leo Machi 20, 2021 ambao waliokuwa wametoka maeneo mbalimbali na wote wakiwa na hamu ya kushuhudia shughuli mbalimbali za kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk.Magufuli .

Mwili wa Dk.Magufuli ulifikishwa Uwanja wa Uhuru saa nne asubuhi ukitokea Kanisa la St.Peters, Dar es Salaam ambako ibada maalum ya kumuaga ilifanyika kabla ya wananchi na viongozi kutoa heshima zao za mwisho katika uwanja huo.

Hata hivyo kote ambako mwili wa Dkt.Magufuli umepitishwa maelfu ya wananchi walikuwa barabarani ambapo wananchi walishindwa kabisa kuwa na ustahimilivu kwani asilimia kubwa ya wananchi hao walionekana wakibubujikwa na machozi kutokana na mapenzi makubwa waliyokuwa wanayo kwa Dkt.Magufuli .

Kabla ya wananchi wakiongozwa na viongozi kuanza kutoa heshima zao za mwisho ibada maalum ilifanyika uwanjani hapo na wakati wa ibada hiyo mengi yamezungumzwa kuhusu Dkt.Magufuli.