Dodoma FM

Mafuriko yakata mawasiliano Vijiji vya Mahama na Nzali

12 January 2021, 12:46 pm

Na,Alfred Bulahya,

Dodoma.

Wananchi wa Vijijini vya Mahama na Nzali katika Kata ya Chilonwa Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, wametakiwa kuacha kutumia barabara inayopita katika mto Nyasungwi unaounganisha Vijiji hivyo ili kuepusha hatari ya kusombwa na maji yaliyojaa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Hayo yamesemwa leo na Diwani wa Kata ya Chilonwa Bw.Alpha Gilbat Msuza wakati akizungumza na Taswira ya habari ambapo amesema kutokana na mto huo kujaa maji tangu mvua zilipoanza kunyesha watumiaji wa barabara hiyo wanapaswa kuacha kuitumia ili kuwa salama.

Aidha amesema kwa sasa viongozi wa Kata kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge na Tanroads wamepanga kuweka bomba zitakazosaidia kupunguza changamoto iliyopo wakati wakisubiri ujenzi wa daraja kubwa utakaokuja kumaliza kabisa tatizo hilo.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni daraja hilo limekuwa ni changamoto kutokana na kujaa maji ambapo januari 1 mwaka huu watu sita walipinduka wakati wakivuka kwa kutumia usafiri wa trekta na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine watano wakiokolewa.