Dodoma FM

Wananchi wahitaji Elimu juu ya zoezi la anuani za makazi

30 March 2022, 3:25 pm

Na; Neema Shirima.  

Wananchi Mkoani Dodoma wameiomba serikali kutoa elimu zaidi juu ya zoezi la anuani za makazi maarufu kama postkodi ambalo linaendelea kwa sasa katika kata zote za mkoani hapa.

Taswira ya habari imefika katika katika mtaa wa Itega kata ya Nkuhungu ambapo zoezi hilo limekamilika jana lakini baadhi ya wananchi kulalamika kutokueleweshwa zaidi juu ya zoezi la anuani za makazi na kuiomba serikali itoe elimu zaidi juu ya zoezi hilo

Bwn Joel Mwanginde ni mwenyekiti wa shina namba tatu katika mtaa wa itega yeye amesema changamoto wanayokutana nayo katika ziara ya kuwaelimisha watu kuhusiana na zoezi la anuani za makazi ni watu kuhusisha zoezi hilo na zoezi na sensa hivyo ameiomba serikali iongeze elimu ili wananchi waweze kutofautisha kati ya zoezi la anuani ya makazi na sensa ya watu na makazi

Aidha kwa upande wa mwenyekiti wa mtaa huo bwana Casian Mponela amesema katika zoezi hilo changamoto kubwa ilikuwa ni kwenye maeneo ambayo hayajapimwa lakini kwa wananchi ambao hawakuwepo majumbani mwao wakati wa zoezi tayari watendaji wa zoezi hilo walishaelekezwa cha kufanya ikiwa hawatawakuta wahusika hivyo wasiwe na wasiwasi kuhusu zoezi hilo.

Serikali inao wajibu wa kuhakikisha inatoa elimu kwa jamii juu la mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo ili wananchi wajitokeze katika ushiriki wa mambo hayo.