Dodoma FM

Jamii yaaswa kuacha unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu

3 December 2020, 3:18 pm

Jaji mstahafu Mathew Mwaimu

Na Alfred Bulahya,

Dodoma.

Tume ya haki za binadamu na utawala bora (THBUB) imewataka wananchi kuachana na mila,desturi pamoja na mitazamo potofu ambayo huwafanya watu wenye ulemavu kuvunjika moyo na kujiona hawana mchango kwa jamii.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na mwenyekiti wa Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji mstaafu Mathew Mwaimu wakati akitoa tamko mbele ya waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu.
Pamoja na hayo ameiomba serikali kuwatumia vyema wataalamun wake kutoa elimu kwa jamii kuhusu ulemavu usioonekana, ambao athari zake zinaweza kumuathiri mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha jaji Mwaimu amesema tume ya haki za binadamu na utawala bora kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutetea haki za watu wenye ulemavu na kuweka msukumo wa utekelezaji wa sheria namba 9 ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 na miongozo ya kimataifa na kikanda.
Katika hatua nyingine Jaji Mwaimu ametoa rai kwa serikali kuendeleza juhudi za makusudi katika kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanawekewa mazingira mazuri ya kupata mahitaji yao kulingana na hali zao.
Chimbuko la siku hiyo linatokana na azimio la baraza kuu la umoja wa mataifa namba 47/3 la mwaka 1992 ambalo liliipitisha Desemba 3 ya kila mwaka kuwa ni siku ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu duniani, ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika wilayani Kongwa Mkoani Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo “si kila ulemavu unaonekana.”