Joy FM

DAS Kasulu ataka vijana kuchangamkia fursa kuinua uchumi wao

26 October 2026, 13:34

Vijana walioshiriki katika mdahalo huo,Picha na Hagai Ruyagila

Vijana ni nguvu kazi muhimu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, wana nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kutokana na nguvu, ubunifu na uwezo wao wa kujifunza mambo mapya na ili waweze kufikia malengo yao na kuboresha maisha yao, wanapaswa kujifunza namna ya kutambua na kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mazingira yao

Na Hagai Ruyagila

Vijana kutoka wilaya za Kasulu na Kibondo mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Hayo yameelezwa na Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtelewe, wakati akimuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo kwenye mdahalo unao waweka pamoja vijana katika kujadili changamoto na fursa ili kuwafanya kuwa sehemu ya maendeleo katika mkoa wao.

Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtelewe, Picha na Hagai Ruyagila

Amesema ni muhimu kwa vijana kuzitambua na kuzichangamkia fursa hizo ili kujipatia kipato na kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, licha ya changamoto ya upatikanaji wa ajira.

Mratibu wa Jukwaa la Vijana kutoka Shirika la ActionAid, Arif Fazel, amesema mdahalo huo umelenga kuwaunganisha vijana ili kujadili changamoto zinazowakabili, kutambua fursa zilizopo na kupata uelewa wa namna ya kuzitumia kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Mratibu wa Jukwaa la Vijana kutoka Shirika la ActionAid, Arif Fazel, Picha na Hagai Ruyagila

Naye Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mikamba Bakari, amezungumzia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika halmashauri hiyo, akitaja sekta ya kilimo kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa kwa vijana kujipatia kipato.

Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mikamba Bakari, Picha na Hagai Ruyagila

Baadhi ya vijana walioshiriki katika mdahalo huo wamesema wamejifunza mambo mbalimbali yatakayowasaidia kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao na kuzitumia kwa ufanisi ili kujikwamua kiuchumi na kufikia malengo yao ya maendeleo.

Jumla ya Vijana 150 kutoka wilaya za Kasulu na Kibondo wamejitikeza kushiriki mdahalo huo uliofanyikia Kasulu Mjini.