Joy FM
Joy FM
29 June 2026, 08:53

Serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na changamoto zao zinatatuliwa kwa wakati na mojawapo ya njia zinazosaidia kufanikisha jambo hili ni viongozi kuwafikia wananchi moja kwa moja, kusikiliza maoni yao na kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, amefanya ziara katika Kata ya Uvinza kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mh. Dinah amesema changamoto ya mabasi kutofika stendi ya mwisho imepata ufumbuzi kufuatia kuanza rasmi kwa shughuli katika Stendi ya Wilaya ya Uvinza. Ameagiza mabasi yote yaliyosajiliwa kutoa huduma hadi Uvinza kuhakikisha yanafika katika stendi hiyo kuanzia leo.
Kwa upande wa maendeleo ya kijamii, Mkuu wa Wilaya amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itatenga na kuandaa eneo linalofaa kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani, ili kukuza ustawi wa jamii na vipaji vya vijana.
Aidha, amewataka maafisa wa Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia haki, sheria na misingi ya utawala bora ili kuimarisha uhusiano mwema kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

Akizungumzia mgogoro wa ardhi unaoikabili Kata ya Ruchugi, Mh. Dinah ameahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa suluhisho la kudumu kwa maslahi ya wananchi wote.
