Joy FM

Biashara na uwekezaji chachu ya maendeleo Kigoma

16 April 2026, 8:08 am

Baadhi ya viongozi mbalimbali wakiwa katika kongamano la uwekezaji ziwa Tanganyika, Picha na Lucas Hoha

Kongamano la biashara na uwekezaji ni chachu ya maendeleo ya Kigoma kwa sababu linafungua milango ya uwekezaji, linaimarisha biashara, na kuongeza ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema mkoa una fursa nyingi za kiuchumi ambazo bado hazijatumika kikamilifu na kuleta tija ya kiuchumi kwa wananachi na taifa kwa ujumla.

Amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na uwepo wa maeneo toshelevu ya kilimo cha mazao ya biashara na chakula, maeneo ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali, vivutio vya utalii na rasilimali madini.

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akizungumza wakati wa kongamano la biashara na uwekezaji, Picha na Lucas Hoha

Balozi Sirro ametoa kauli hiyo alipozungumza wakati akifungua Kongamano la biashara na uwekezaji Ziwa Tanganyika, linalofanyika Mkoani hapa Aprili 15 hadi 16, ambapo mgeni Rasmi katika  kilele chake anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Amesema Mkoa una fursa za uwepo wa maeneo kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya Parachichi, chikichi, muhogo sambamba na uwepo wa rasilimali ya kimkakati ya ziwa Tanganyika ambalo linachangia kiasi kikubwa uzalishaji wa mazao ya uvuvi.

Aidha,  amesema kwa sasa mkoa umeunganishwa na mikoa jirani kwa barabara za Lami, Uwepo wa umeme toshelevu, usafiri wa uhakika wa anga sambamba na kuanza kwa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR,  ambayo itauunganisa mkoa na nchi jirani ya Burundi.

Baadhi ya viongozi wakuu waliohudhuria kongamano la biashara na uwekezaji, Picha na Lucas Hoha

Kupitia Kongamano hilo, balozi Sirro amewaalika wawekezaji kutoka ndani na nje ya Mkoa kuzitazama fursa hizo zilizopo mkoani hapa kwa ajili ya kufanya uwekezaji na kutoa ajira kwa wananchi sambamba na kushusha bei ya bidhaa mbalimbali.

Aidha amesisitiza kuwa lengo la kongamano hilo ni kuonesha kwa vitendo uwepo wa fursa za kiuchumi na uwekezaji mkoani Kigoma na kujenga mahusiano ya kimkakati katika uwekezaji kwa Maendeleo ya nchi na jumuia ya Afrika Mashariki kwa ujumla.