Joy FM

SACP Makungu ataka wananchi kudumisha amani Kibondo

31 July 2026, 15:45

Baadhi ya askari Polisi wakitoa damu ikiwa semehu ya maadhimisho ya siku ya Polisi, Picha na Dotto Josephati

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma SACP Filemoni Makungu amewataka wananchi Mkoani Kigoma kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na wahalifu

Na Dotto Josephati

Wananchi Mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kudumisha amani na kushirikiana katika maeneo yao ili kuhakikisha vitendo vya uhalifu na ukatili havitokei katika jamii.

Wito huo umetolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Filemon Makungu, wakati wa zoezi la kufanya usafi wa mazingira na kuchangia damu katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Filemon Makungu, Picha na Dotto Josephati

Shughuli hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Polisi Jamii, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

SACP Makungu amesema kuwa katika maadhimisho ya wiki hiyo, Jeshi la Polisi limejikita kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika masuala ya ulinzi na usalama wa maeneo yao.

Baadhi ya askri Polisi Wilayani Kibondo wakifanya usafi wa mazingira, Picha na Dotto Josephati

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, Dkt. Cornnely Nibiki, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kushiriki katika shughuli hizo ambapo amesema damu iliyochangwa itasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu katika hospitali hiyo.

Katika zoezi hilo, jumla ya uniti 34 za damu zimekusanywa kutoka kwa askari polisi, hatua inayotarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.