Joy FM

Serikali imesema inatambua mchango wa taasisi za dini Kasulu

30 July 2026, 10:28

Picha ya pamoja Katibu tawala wa Wilaya ya Kasulu akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma balozi Simon Sirro na viongozi wengine wa dini wakati wa ibada ya kumsimika askofu mpya wa Jimbo la Kigoma, Alex Kalalaye, Picha na Hagai Ruyagila.

Viongozi wa dini wametakiwa kuendelea kuhimiza jamii na waumini wao kusimamia maadili mema ili kuwa kizazi chema

Na Hagai Ruyagila

Serikali ya Mkoa wa Kigoma imesema inaendelea kutambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika kujenga taifa lenye maadili mema, kuhamasisha wananchi kudumisha amani na upendo, hali inayowezesha Serikali kutekeleza kwa ufanisi mipango yake ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, Afya pamoja na elimu

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtelewe, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, wakati wa ibada takatifu ya kumsimika Askofu wa Kanisa la HOFAN Jimbo la Kigoma, Askofu Alex Kalalaye, iliyofanyika Mjini Kasulu.

Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtelewe, Picha na Hagai Ruyagila

Bi. Mtelewe amesema mafanikio yanayopatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yanahitaji kuungwa mkono na wananchi pamoja na viongozi wa dini kwa kuendelea kuhubiri amani, uzalendo na uwajibikaji ili kujenga jamii yenye maadili mema.

Sauti ya Bi. Theresia Mtewele

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu sheria za nchi, kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuwaombea viongozi wa dini ili taifa liendelee kuwa na amani.

Sauti ya Bi. Theresia Mtewele

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la HOFANI Taifa, Dkt. Charles Jangalason, amewasisitiza viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kuishi maisha yenye maadili mema yatakayochochea upendo, amani, mshikamano na maendeleo endelevu katika jamii.

Sauti ya Askofu Dkt Charles Jangalason
Askofu Mkuu wa Kanisa la HOFANI Taifa, Dkt. Charles Jangalason, Picha na Hagai Ruyagila

Naye Askofu mpya wa Kanisa la HOFANI Jimbo la Kigoma, Askofu Alex Kalalaye, ameahidi ushirikiano wa karibu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kujenga waumini kuwa raia wema, wachapakazi na wenye mchango chanya katika maendeleo ya taifa.

Sauti ya Askofu Alex Kalalaye
Askofu mpya wa Kanisa la HOFANI Jimbo la Kigoma, Askofu Alex Kalalaye, Picha na Hagai Ruyagila