Joy FM
Joy FM
19 June 2026, 22:06

Mpango huo umetajwa na kuwa na manufaa kwa wakulima iwapo utasimamiwa vizuri na kuhakikisha wakulima wanapata faida
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, ameongoza kikao cha wadau wa zao la pamba kilichofanyika Juni 19, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kwa lengo la kujadili maandalizi ya ununuzi wa pamba kwa msimu wa 2025/2026.
Kikao hicho kiliwakutanisha wawakilishi wa wakulima, wanunuzi, viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), maafisa ugani pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za kilimo. Wadau hao walijadili masuala ya bei ya pamba, ubora wa zao, matumizi sahihi ya mizani na changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa ununuzi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mh. Dinah amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha wakulima wananufaika na jasho lao. Aidha, alielekeza tathmini ya bei ya pamba izingatie gharama halisi zinazobebwa na mkulima katika uzalishaji wa zao hilo.
“Serikali inataka kuona wakulima wananufaika na hakuna mkulima anayepaswa kudhulumiwa kupitia mizani isiyo sahihi au ucheleweshaji wa malipo,” alisema Mh. Dinah.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Uvinza , Ndg. James Mkumbo aliwataka maafisa ugani kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na wavunaji wa pamba kuhusu kuzingatia viwango vya ubora ili waweze kupata bei nzuri sokoni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Kaimu Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo, Ndg. Japheth Njawala, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha mkulima wa pamba ananufaika zaidi kupitia uwekezaji wa kampuni ya NGS, ambayo imeanzisha kiwanda katika Kijiji cha Chakulu kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa pamba na upatikanaji wa masoko.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza za kuimarisha sekta ya kilimo na kuhakikisha zao la pamba linaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo.