Joy FM
Joy FM
24 June 2026, 09:16

Maendeleo yanategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa taasisi za Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kufanikisha hilo, ni muhimu kuwa na vitendea kazi vya kutosha na vinavyokidhi mahitaji ya kazi
Na Mwandishi wetu
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibondo, Bi. Upendo Marango, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Mhe. Aggrey Magwaza, amezindua gari jipya aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili SM 44794 kwa ajili ya Idara ya Mipango. Gari hilo limenunuliwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa lengo la kuimarisha utekelezaji, ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Bi. Upendo Marango alisema kuwa upatikanaji wa gari hilo ni hatua muhimu inayoonesha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.

Ameeleza kuwa gari hilo litawezesha maafisa wa Idara ya Mipango kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kufanya tathmini za mara kwa mara, pamoja na kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaendana na malengo yaliyokusudiwa.
“Serikali inaendelea kuwekeza katika vitendea kazi ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa viwango vinavyotarajiwa,” alisema Bi. Upendo Marango.

Aidha, aliwataka watumishi watakaolitumia gari hilo kulihudumia na kulitunza ipasavyo, pamoja na kulizingatia matumizi sahihi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Serikali, ili liweze kudumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Diocles Rutema, alisema kuwa gari hilo litakuwa nyenzo muhimu katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, zikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu na maendeleo ya jamii.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa gari hilo utaongeza ufanisi wa kazi za Idara ya Mipango na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo yaliyowekwa kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Kibondo.