Joy FM

Rushwa ya ngono yawaliza wanawake wachuuzi wa samaki Kigoma

10 June 2026, 16:31

Wauzaji wa samaki katika mwalo wa Kibirizi Manispaa ya Kigoma, Picha na Mtandao

Rushwa ya ngono imeendelea kuwa mwiba kwa wanawake katoka maeneo mbalimbali ya utafitaji wa wanawake kitu ambacho kimeendelea kuwarudisha nyuma na kushindwa kufikia ndoto zao

Na Timotheo Leonard

Wanawake wachuuzi wa samaki katika Soko la Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji, wameeleza kukabiliwa na vitendo vya rushwa ya ngono wanapotekeleza shughuli zao za kila siku za biashara.

Wakizungumza na Joy Fm, wanawake hao wameomba mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo hivyo ambavyo vimeendelea kuathiri maisha na biashara zao.

Kwa nyuso zenye matumaini ya maisha bora lakini zilizobeba simulizi za maumivu, wanawake hawa wachuuzi wa samaki wanasema rushwa ya ngono imeendelea kuwa mzigo unaowakandamiza.

Wanaeleza kuwa vitendo hivyo vinakiuka utu wao na kuathiri jitihada zao za kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa soko hilo anasema ni muhimu wanawake kuendelea kusimama imara na kutokubali kushinikizwa kufanya vitendo vinavyokiuka haki zao

Mkuu wa dawati la elimu kwa umma takukuru mkoa wa Kigoma , amesema rushwa ya ngono ni aina ya rushwa inayotambuliwa kisheria na ni kosa linalostahili hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2024 iliyotolewa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Polisi pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, idadi ya wahanga wa ukatili wa kingono imeongezeka kwa asilimia 30.1, kutoka wahanga 11,028 mwaka 2022 hadi kufikia wahanga 14,354 mwaka 2023.

Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kigoma Ujiji Dawati la msaada wa kisheria Bi Salome Munyi amesema vitendo vya rushwa ya ngono Vipo na huacha athari kubwa kwa waathirika, ikiwemo msongo wa mawazo, kupoteza kujiamini, kudhoofika kwa afya ya akili pamoja na kuathiri ustawi wa kijamii na kiuchumi na hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa wavuvi,wanawake wachuuzi na jamii yote.

wanawake hawa zinavyoendelea kusikika, ujumbe wao unabaki kuwa mmoja; kuvunja ukimya, kutoa taarifa na kushirikiana na vyombo vya sheria ili kutokomeza rushwa ya ngono. Kwa sababu rushwa ya ngono si tu kwamba inakiuka sheria za nchi, bali pia inanyima wanawake haki, heshima na fursa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Lakini je Wanawake na jamii kwa ujumla wanafahamu mazingira au viashiria vya rushwa ya ngono?Wanafahamu wapi pa kupeleka malalamiko?Afisa wa Dawati la Jinsia wanawake na watoto Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma Mrakibu msaidizi wa Polisi Michael Mjema anabainisha.

Rushwa ya ngono ni moja ya changamoto kubwa hasa kwa jamii ya Wanawake ambao ni wahanga wakubwa na mwarobaini wake umeonekana kuwa mgumu kutokana na uelewa duni,Hofu ya kukosa fursa au vinginevyo.