Joy FM
Joy FM
27 May 2026, 13:13

Msaada huo unasaidia kuboresha afya za wanafunzi wenye mahitaji maalum kupitia bima hizo, wanafunzi wataweza kupata huduma za matibabu kwa urahisi wanapougua au wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kiafya
Na Hagai Ruyagila
Taasisi ya Usilie Tena kutoka jijini Dar es Salaam imetoa bima za afya kwa wanafunzi 66 pamoja na pea 400 za viatu aina ya Yeyo Yebo kwa wanafunzi wa shule za msingi ikiwemo Titye, Kisuma na katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, kwa lengo la kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum kupata huduma za matibabu wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kiafya.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa bima hizo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Usilie Tena, Bi. Egla Kamugisha, amesema wameamua kutoa msaada huo ili kuwasaidia wanafunzi hao kupata huduma za afya kwa urahisi na kuwawezesha kuendelea na masomo yao bila vikwazo vinavyotokana na matatizo ya kiafya.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Isaac Mwakisu, ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa bima hizo za afya ambazo zitawasaidia zaidi watoto wenye mahitaji maalumu. Pia amewasisitiza wazazi kuzitunza bima hizo ili ziweze kuwasaidia watoto wao ipasavyo pale wanapohitaji huduma za matibabu.

Kwa upande wake, mdau wa elimu maalum Mwl. Yusuph Ibrahimu kutoka Shule ya Msingi Kisuma amesema kwasasa muamko wa wazazi kuwapeleka watoto shule umeongezeka kutokana na elimu inayotolewa na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa elimu.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Titye Hilal Abdallah amesema msaada huo utapunguza sana changamoto kwa wazazi kugharamia matibabu ya watoto wao.

Baadhi ya Wazazi wa wanafunzi walionufaika na bima hizo wameeleza furaha yao kwa msaada huo, kwamba utawasaidia kupata matibabu bila usumbufu wowote.