Joy FM

Wananchi wajitolea kutengeza barabara Buhigwe

29 April 2026, 09:18

Wakazi wa kitongoji cha Janda Juu kata ya Janda Wilayani Buhigwe, Picha na Mwandishi wetu

Katika maeneo mengi ya Tanzania, hii huonekana kama nguvu kazi ambapo wananchi hukusanyika kusafisha, kujaza mashimo, au hata kuchimba mitaro na kutengeneza barabara ili kurahisha usafiri na usafirishaji

Na Mwandishi wetu

Wakazi wa kitongoji cha Janda Juu kata ya Janda Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wamejitolea kutengeneza barabara itakayowasaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani pamoja na kusaidia wakazi wa eneo la Kilulu kupata huduma mbalimbali kwa urahisi ikiwemo Elimu na huduma za afya.

Wakizungumza wakati wa zoezi la utengenezaji wa barabara hiyo, baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho akiwemo Joseph Chiha na Angela Kassim wameeleza kuwa ukosefu wa barabara hiyo umekuwa changamoto kubwa inayokwamisha upatikanaji wa huduma muhimu hususani kwa wakazi wa eneo la Kilulu ndani ya kitongoji hicho.

Baadhi ya wananchi wakiwemo wanawake wakiwa katika utengenezaji wa barabara, Picha na Mwandishi wetu

Mwenyekiti wa kitongoji cha Janda Juu, Damas Lugigidi amesema kuwa juhudi za wananchi kujitolea kutengeneza Barabara hiyo zinaonesha namna walivyo tayari kushirikiana katika kuleta maendeleo ya eneo lao, huku akiiomba serikali kuunga mkono jitihada hizo ili kuhakikisha barabara hiyo inaboreshwa zaidi na kudumu kwa muda mrefu.

Mwakilishi wa mwenyekiti wa kitongoji cha Janda Juu katika eneo la Kilulu, Ernest Daniel amesema kuwa kukosekana kwa Barabara hiyo kumekuwa kikwazo kikubwa kwa wakazi eneo kufikia huduma za msingi ikiwemo Elimu na huduma za afya.

Baadhi ya wananchi wakiwemo wanawake wakiwa katika utengenezaji wa barabara, Picha na Mwandishi wetu

Aidha Diwani wa kata ya Janda Wilayani Buhigwe Shabani Seleman amesema kuwa ameshawasilisha changamoto ya barabara hiyo katika mamlaka husika ili kuona uwezekano wa kutengenezwa kwa kiwango bora ili kuwahudumia wananchi wa eneo hilo.

Sauti ya Mwandishi wetu