Joy FM
Joy FM
23 July 2026, 09:22

Serikali imeendelea kuboresha na kupanua mtandao wa barabara Mkoani Kigoma kwa lengo la kuhakikisha suala la usafiri na usafirishaji linaimarishwa.
Na Mwandishi wetu
Wananchi wa Wilaya ya Kakonko wanatarajia kunufaika na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuelekea Makao Makuu ya Serikali baada ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, kuahidi utekelezaji wa mradi huo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Waziri Ulega alianza ziara yake kwa kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Kakonko, ambapo alisaini kitabu cha wageni na kupokea taarifa fupi ya maendeleo ya wilaya. Baadaye alitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko na kuzungumza na watumishi, akiwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, aliwataka kutumia fursa zilizopo Kakonko kushiriki shughuli za uzalishaji na uwekezaji zitakazowaongezea kipato na kuchochea maendeleo ya eneo hilo.Katika ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kakonko, Mhe. Allan Mvano, aliwasilisha ombi la kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara, hususan barabara inayounganisha eneo la mjini na Ofisi za Halmashauri pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Alieleza kuwa ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami utarahisisha shughuli za kiutawala, kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza hadhi ya Makao Makuu ya Wilaya.
Akijibu ombi hilo, Waziri Ulega aliahidi kuwa Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami na kubainisha kuwa tayari ametoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma kuanza taratibu za utekelezaji.
Alisisitiza kuwa ujenzi huo utaimarisha miundombinu ya wilaya, kurahisisha utoaji wa huduma za Serikali na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Kakonko.